Klabu ya Azam FC imetoa sababu kwa nini imekua kwenye harakati za kuhakikisha inamaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu msimu wa 2019/20, ambao mwishoni mwa juma hili utafika ukingoni.
Azam FC ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama 66 inapambania nafasi ya pili ambayo ipo mikononi mwa Young Africans yenye alama 69 jambo linaloongeza ushindani wa nafasi.
Azam FC leo Al-Khamis itashuka dimbani kucheza mchezo wa 37 wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City FC, Uwanja wa Azam Complex Chamazi, jijini Dar es salam.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Azam FC Thabit Zakaria (Zaka Zakazi), amesema kuwa malengo ya klabu ni kuona yanatimia kwa kumaliza kwenye nafasi ya pili ambayo kwao ni sehemu ya rekodi.
“Tulianza na malengo ya kufikiria ubingwa ukapotea, tukaongeza malengo ya kuwa nafasi ya pili sababu kubwa kuhitaji nafasi hii ni heshima pamoja na rekodi kwani kuna wakati unatazama msimu fulani ukiwa wapi na ulifanya nini kwetu ni mafanikio pia.
“Kitu pekee kilichobaki kwa sasa kwetu ni kuangalia makosa yetu na kupambana kushinda mechi zetu kwani tuna mchezo na Mbeya City nao ni mgumu hivyo bado tunasubiri kuona mambo yatakuaje,” amesema Zakaria.
Kwenye mchezo wa leo mbele ya Mbeya City, Azam FC itakosa huduma ya beki Nicolas Wadada ambaye ana kadi tatu za njano.