Mpambano wa Alliance FC dhidi ya Ndanda FC utakaochezwa baadae hii leo, unatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na timu hizo kuwa kwenye hali mbaya ya kushuka daraja.

Katika msimamo wa Ligi Kuu timu ya Ndanda FC inashika nafasi ya 18 ikiwa na alama 40 huku Alliance FC wakishika nafasi ya 17 kwa alama 41, wote wakicheza mechi 36.

Akizungumzia mchezo huo utakaoanza mishale ya saa kumi jioni kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, Kocha mkuu wa Alliance FC Kessy Mziray amesema, utakuwa mchezo mgumu kwa kila timu.

Mziray amesema, ugumu wa mchezo huo unatokana na timu zote kuwa katika hatari ya kushuka daraja, hivyo kila mmoja anapamba ashinde.

“Mchezo utakuwa ngumu sana, kama ambavyo unaona katika msimamo wote hatuko kwenye hali nzuri tuko nafasi mbaya, hivyo tunahitaji matokeo na Ndanda pia wanahitaji matokeo hapo tunamuachia Mungu,” amesema Mziray

Mziray amesema, dakika 90 za mpambano huo ndizo zitaamua, huku akijinasibu kuutumia vyema uwanja wa nyumbani ili kujiongezea alama.

“Nimewaambia wachezaji wapambane kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo ili tujiweke nafasi nzuri ya kuepuka kushuka daraja,” amesema Mziray

Amesema kikosi chake kipo vizuri na tayari kwa mchezo huo kwani atamkosa mchezaji mmoja tu Wema Sadoki ambaye aliumia kifundo cha mguu hivi karibuni.

Dodoma: Kiongozi wa CHADEMA auawa kwa mshale
Wavuvi Kigamboni walia na kanuni mpya