Ni kama shangwe la Azam FC kuifunga Simba SC linaendelea katika viunga vya Azam Complex, Chamazi baada ya kiongozi wa juu wa klabu hiyo kukiri wamefurahishwa na kilichotokea mkoani Mtwara Jumapili (Mei 07) kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Azam FC ilifanikiwa kutinga Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa kuifunga Simba SC 2-1 katika mchezo wa Nusu Fainali ambao ulichezeshwa na Mwamuzi Tatu Malongo kutoka jijini Tanga.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulkarim Nurdin Amin ‘Popat’ amesema ni furaha kubwa kwao kuifunga Simba SC zaidi ya mara moja msimu huu, hali ambayo imedhihirisha ubora wa kikosi chao na namna walivyojipanga kutimiza malengo waliojiwekea.

“Ni fahari kubwa sana kuwachapa hawa jamaa (Simba SC), wametusumbua sana lakini msimu huu kwenye ligi tumewachapa na FA tumewachapa”

Kuhusu furaha yao kuhusishwa na upande wa Young Africans Popat amesema wanajua hilo lipo, kwa sababu ziku zote madhaifu ya Simba SC ni furaha kwa Wananchi, pamoja na wao hawatapendezwa kuona Azam FC ikitwaa Ubingwa.

“Mashabiki wa Young Africans wanatamani tuwaumize Simba ila hawako tayari Azam FC iwe bingwa, wanataka tuwe nafasi ya pili, hivyo hivyo hata kwa mashabiki wa Simba SC” amesema Popat

Azam FC inamsubiri mshindi wa Nusu Fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ ambayo itachezwa mjini Singida Mei 21 kati ya Mabingwa watetezi Young Africans dhidi ya Singida Big Stars.

CEO Simba SC afafanua posho za wachezaji
Dabalo wafaidi Milioni 600 za UNFPA