Baada ya kuonja shubiri ya kupoteza alama tatu kwa mara ya kwanza msimu huu 2020/21 dhidi ya Mtibwa Sugar, Uongozi wa Azam FC umekiri wababe hao wa Morogoro hawakuwa fungu lao.
Azam FC ilipoteza mchezo huo jana Jumatatu Oktoba 26, Uwanja wa Jamuhuri mkoani Morogoro kwa kufungwa bao moja kwa sifuri, lililofungwa na mshambuliaji Jaffar Kibaya dakika ya 62.
Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya Azam FC Zakaria Thabit amesema:-“Wachezaji wamefanya kazi nzuri mwisho wa siku matokeo hayakuwa upande wetu. Tumepoteza mchezo wetu wa kwanza kwa msimu wa 2020/21.
“Bado ni sehemu ya mchezo na tutaendelea kupambana kwani haikuwa fungu letu la kushinda tunajipanga kwa ajili ya mechi zijazo, tuna kikosi kizuri na wachezaji wapo vizuri.”
Kwenye mchezo wa jana ni nyota wawili wa kikosi cha kwanza walikosekana ambao ni Obrey Chirwa abaye ni mshambuliaji mwenye mabao manne alikuwa anasumbuliwa na maumivu ya enka.
Salum Abubakar, Sure Boy alikuwa ana adhabu ya kadi tatu za njano, yeye ana pasi moja ya bao.
Azam FC inayonolewa na kocha kutoka nchini Romania Aristica Cioaba ilikuwa imecheza jumla ya michezo saba bila kupoteza tangu mwanzoni mwa msimu huu 2020/21.
Azam FC bado ipo nafasi ya kwanza ikiwa na alama 21 baada ya kucheza michezo minane, Mtibwa Sugar imejisogeza hadi kwenye nafasi ya 10 ikiwa na alama 11 nayo imecheza michezo.