Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuanzisha Ligi ya Vijana chini ya umri wa miaka 15 (Azam Youth League U-15), itakayoanza kutimua vumbi kuanzia Oktoba 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Ligi hiyo inakua ya pili kwa vijana baada ya ile ya chini ya umri wa miaka 13 (Azam Youth League U-13) iliyomalizika Julai mwaka huu ikishuhudiwa Bom Bom FC ikiwa mabingwa na Azam U-13 ikishika nafasi ya tatu.
Akitangaza ligi hiyo Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana Azam FC, Tom Legg, alisema kuwa ligi hiyo itakuwa ikifanyika kila Jumamosi kwa muda wa wiki kumi huku akizitaja timu zinazoshiriki kuwa ni Bom Bom SC, JMK Park Academy, Rendis FC, New Talent na Florida Academy.
“Kwa muda wa wiki 10 timu zitacheza nyumbani na ugenini, ligi ya U-15 itahusisha wachezaji 11 dhidi ya 11 tumeziboresha baadhi ya kanuni ili kuhakikisha kuwa wachezaji wanacheza na vilevile kujifunza ndani ya wiki hizo 10,” alisema.
Alisema kuwa kama walivyofanya kwenye michuano iliyopita kudhibiti umri wa wachezaji, pia safari hii wamejipanga vilivyo kuhakikisha wachezaji wote wanaocheza michuano hiyo wanakuwa kwenye umri unaotakiwa wa chini ya miaka 15.
“Kila mchezaji atayeshiriki michuano hiyo atapimwa na mimi na baadhi ya watu wa benchi la ufundi katika siku ya usajili, kila mchezaji atatakiwa kuonyesha nakala ya cheti chake cha kuzaliwa au uthibitisho wowote na taarifa zote zitawekwa mtandaoni na kila kocha wa timu zote ataweza kujionea taarifa hizi,” alisema.
Legg alisema kuwa wanatarajia kuitanua ligi hiyo Tanzania nzima kwenye vituo vyao maalumu watakavyovianzisha hapo baadaye ikiwa ni mipango ya muda mrefu, lakini katika mipango ya muda mfupi wameamua kuanza na mkoa wa Dar es Salaam.
Katika kujiandaa na ligi hiyo, tayari kikosi cha Azam FC U-15 kinaendelea na mazoezi makali kila siku za Jumanne, Alhamisi na Jumamosi, ikicheza mechi za kujipima ubavu.