Uongozi wa Klabu ya Azam FC umesema uko tayari kumuuza kiungo wao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kwa Young Africans au klabu yoyote inayomuhitaji, endapo wataenda mezani na kuafikiana kuhusu dau la mchezaji huyo.
Sure Boy amecheza kwa mafanikio makubwa katika kikosi cha Azam FC kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10, huku kukiwa na taarifa ya Yanga kuhitaji huduma yake.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema wako tayari kumuuza mchezaji huyo, hivyo wanamkaribisha yeyote anayemtaka.
Hata hivyo imekua kawaida kwa klabu za Simba na Young Africans kuhusishwa na mipango ya usajili wa wachezaji kadhaa unapofika muda kama huu wa kuelekea mwishoni mwa msimu.
“Tunasikia kuwa kuna baadhi ya timu zinamuhitaji mchezaji wetu Salum, sisi tunachojua ni kuwa bado mchezaji huyo ana mkataba na Azam lakini hilo haliondoi uwezekano wa kumpata kwa klabu yoyote inayomuhitaji.
“Unajua kuna wakati wachezaji wanaweza kuvutiwa na mkakati fulani kutoka klabu nyingine jambo ambalo linakubalika, hivyo kama Yanga watakuja mezani tukazungumza na mchezaji mwenyewe akaridhia basi sisi hatuna kipingamizi tutaruhusu aende,” amesema Zaka Zakazi.
Alipotafutwa Afisa Habari wa Young Africans, Hassan Bumbuli alisema: “Kwa sasa niwatoe hofu mashabiki na wapenzi wa Yanga kuwa mambo mazuri yanakuja ila waendelee kuwa na subira kila kitu kitakuwa wazi.
Mara kadhaa klabu hizo kongwe zimekua hazifanyi usajili wa wachezaji wenye mikataba na klabu zao kwa kuhofia gharama kubwa za usajili, na badala yake husubiri mpaka wanapomaliza mikataba yao, ili wawasajili kama wachezaji huru.