Imeelezwa kuwa mabosi wa Azam FC wamemuongezea mkataba wa miaka miwili kiungo wake mkabaji, Sospeter Bajana katika kuelekea usajili mkubwa wa msimu ujao.
Kiungo huyo anayecheza jihad na nguvu nyingi katika nafasi ya namba sita, alikuwa akitajwa katika usajili wa Simba SC kwa ajili ya kuwasaidia Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin.
Simba SC hivi sasa imemfuata kiungo wa St George ya Ethiopia, Gatoch Panom ambaye yeye dau lake la usajili Sh 350 baada ya kupata taarifa kutoka Azam za kumkuongezea mkataba Bajana.
Mmoja wa Mabosi wa Azam FC amesema kiungo huyo ataendelea kubakia hapo katika misimu mingine miwili hadi 2025.
Bosi huyo amesema kuwa kiungo huyo amesaini mkataba huo baada ya uongozi wa Azam FC kumpa dau nono la usajili ambalo limemshawishi aendelee kubakia kukipiga hapo.
“Bajana ameongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia Azam FC hadi Juni 2025. Katika mkataba wake atakuwa akilipwa mshahara unakaribia kufika Sh 10 Milioni.
“Ofa hiyo ameiona nzuri kwake na kuchukua maamuzi ya kubakia kuendelea kubakia hapo, na amelipwa mshahara huo mkubwa kama sehemu ya kumshawishi aendelee kubakia hapo.
“Kwani kama wasingempa mshahara huo, basi angekwenda kusaini Simba ambayo ilikuwa inafahamu mkataba wake na uongozi umeaahidi kutorudia makosa yaliyosababisha kuwaachia baadhi ya wachezaji wao muhimu waliokwenda Simba Bocco (John), Manula (Aishi), Kapombe (Shomari) na Nyoni (Erasto),” amesema bosi huyo.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdoulikarim Karim ‘Popat’ hivi karibuni alithibitisha hilo kwa kusema kuwa: “Kamwe hatutarudia makosa kama tuliyofanya ya kuwaachia wachezaji wetu muhimu kuondoka hapa na kwenda Simba.
“Kikubwa tulijisahau kuwaongezea mikataba mipya na kuchukua maamuzi ya kwenda Simba akina Bocco, Nyoni, Manula na Kapombe, hatutaki hiyo itokee tena, hivyo tutawaongezea mikataba mipya wachezaji wote waliokuwepo katika mipango ya timu.”