Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulkareem Amin ‘Popat’ amesema klabu yao haina mpango wowote wa kumsajili Kiungo wa Young Africans Feisal ‘Fei Toto’.

Kiungo huyo amekua gumzo katika vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii, kufuatia taarifa aliyoiweka katika Ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Instagram mwishoni mwa juma lililopita, akiwaaga Mashabiki, Wanachama na Wachezaji wenzake wa Young Africans na baadae Uongozi kumjibu.

Popat amekanusha taarifa za kuwaniwa kwa Kiungo huyo alipohojiwa na Kituo cha Radio cha Wasafi FM mapema leo Alhamis (Desemba 29), ambapo amesema wanaona na kusikia Klabu yao inatajwa kwenye sakata la Mchezaji huyo, lakini hawana mpango wowote wa kumsajili.

Popat amesema Azam FC inafahamu utaratibu wa kumsajili mchezaji mwenye mkataba na asiye na Mkataba na mara zote imekua inafuata utaratibu wa kikanuni, hivyo inawashangaza sana kuona Klabu yao inaingizwa kwenye Sakata la ‘Fei Toto’.

“Sisi wenyewe tunasoma tu mitandaoni kuhusu Feisal Salum. Hakuna siku tuliyowahi kukaa na kusema tunamtaka Feisal. Yule ni mchezaji mzuri na tegemeo katika timu yake ya Yanga na timu ya taifa.”

“Hakuna timu ambayo haiwezi kumtamani Feisal, lakini sisi kama Azam FC hatuna taarifa ya namna hii maana hakuna sehemu tuliyosema wala kuandika kuwa tunamtaka Feisal “

“Halafu Azam FC tunafahamu namna ya kumsajili Mchezaji mwenye Mkataba na Klabu yake na tumefanya hivyo mara kadhaa, Pia tunajuwa namna ya kumsajili mchezaji ambaye hana Mkataba yaani yupo huru, kwa sasa nini ionekane tunaharibu heshima yetu kwa huyo anayetajwa?” amehoji Popat

Azam FC: Tumepokea ofa ya Young Africans
Mawaziri watatu wajiuzulu akiwemo Naibu Waziri wa Afya