Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nassredine Nabi, anaendelea kuumizwa kichwa kuelekea mchezo wa Mzunguuko watatu wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC.
Miamba hiyo ya Dar es salaam, itakutana Jumanne (Septemba 06), kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, majira ya saa moja usiku.
Kocha Nabi amesema amekua akisaka mbinu za kuikabili Azam FC, kutokana na wapinzani wake kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi, baada ya kusajiliwa wachezaji wengi na wenye uwezo mkubwa msimu huu.
Amesema anafahamu mchezo huo wa Septemba 06, utakuwa ngumu na wenye ushindani mkubwa, hivyo hana budi kupanga mikakati mizito ambayo itamuwezesha kuibuka na alama zote tatu.
“Mabadiliko kwenye kikosi cha Azam FC ni sehemu ambayo inaufanya mchezo huu kuwa mgumu, hata mabadiliko katika Benchi la Ufundi nayo yanaufanya mchezo huo kuwa na changamoto kubwa sana.”
“Mchezo hautakuwa rahisi, ni mchezo muhimu kwetu kupata matokeo, tutaingia tofauti, hatutatumia mbinu ambazo tulizitumia katika mechi zetu za ugenini, tutabadilisha mfumo kwa sababu kila mchezo unahitaji mpango kazi tofauti,”
“Tunajipanga vizuri ili kupata mbinu sahihi za kuikabili Azam FC, kwa sababu tunajua haitakuwa kama msimu uliopita, nimeifuatilia Azam FC nimeona kuna baadhi ya vitu viko tofauti kabisa.” amesema Nabi
Young Africans imeshajikusanyia alama sita, baada ya kushuka dimbani mara mbili, ikiifunga Polisi Tanzania 2-1 na kisha ikaichapa Coastal Union 2-0, michezo yote ikichezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Azam FC nao wameshuka dimbani mara mbili na kujikusanyia alama nne, wakiifunga Kagera Sugar 2-1, na baadae walilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Geita Gold FC, Michezo yote ikichezwa Azam Complex Chamazi, Dar es salaam.