Baada ya kucheza michezo miwili ya Kirafiki katika kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Uongozi wa Azam FC umekiri kuridhishwa na mwenendo wa kikosi chao, kuelekea mchezo wa Mzunguuko watatu dhidi ya Young Africans.

Azam FC itakua mgeni wa Young Africans kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Jumanne (Septemba 03), mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Soka la Bongo.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria amesema baada ya michezo miwili ya Kirafiki waliocheza dhidi ya Taifa Jang’ombe ya Zanzibar na Arta Solar kutoka Djibout, kikosi chao kimeendelea kuimarika.

Thabit amesema kutokana na mabadiliko yanayoonekana huku kikosi chao kikiendelea kujiandaa na mchezo dhidi ya Young Africans, hawana hofu yoyote na wana matumaini makubwa ya kwenda kupambana.

“Kwa hakika tunaona mabadiliko kwenye kikosi chetu, tumecheza michezo miwili ya kirafiki, imetusaidia sana kuwaweka sawa wachezaji wetu,”

“Upande wetu hatuna hofu yoyote, tunasubiri muda ufike, mazoezi yanayoendelea ni ya kuiweka miili ya wachezaji wetu tayari, lakini kiufundi tulishamaliza kazi,” amesema Thabit

Young Africans imeshajikusanyia alama sita, baada ya kushuka dimbani mara mbili, ikiifunga Polisi Tanzania 2-1 na kisha ikaichapa Coastal Union 2-0, michezo yote ikichezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Azam FC nao wameshuka dimbani mara mbili na kujikusanyia alama nne, wakiifunga Kagera Sugar 2-1, na baadae walilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Geita Gold FC, Michezo yote ikichezwa Azam Complex Chamazi, Dar es salaam.

Ibenge aihofia Young Africans Ligi ya Mabingwa Afrika
Azam FC yamvuruga Nassredine Nabi