Kocha Msaidizi wa Pamba Jiji FC Renatus Shija, amependekeza uongozi wa klabu hiyo kuanza maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao mapema kwa kutoa fungu la kusajili wachezaji wapya, pamoja na kuwalinda waliopo wasiondoke huku akiwataka mashabiki wa soka Mwanza kuwa watulivu.

Kocha huyo amesema Ligi Kuu Tanzania kwa sasa imebadilika kwani ina ushindani mkubwa, hivyo maandalizi ya mapema yanatakiwa ili kuifanya Pamba kuwa timu ya ushindani.

“Tumeshapanda Ligi Kuu, huu sasa siyo wakati wa maneno maneno, wakazi wa Mwanza watulie, Pamba inahitaji maandalizi ya mapema, tunakwenda kwenye Ligi Kuu huko ushindani ni mkubwa zaidi, menejimenti iweke fungu la usajili, pamoja na la kuwalinda wachezaji, kwa sababu ushindani ni mkubwa wa kugombea wachezaji.”

“Hatuwezi kuingia moja kwa moja na kuweka ushindani mkubwa moja kwa moja, lazima kwanza tuizoee ligi,” amesema kocha huyo aliyepandisha Pamba Jiji kwa mara ya kwanza baada ya miaka 23.

Katika mechi hiyo, timu hizo ambazo zote zimepanda Ligi Kuu, zilitoka sare ya bao 1-1 na KenGold kupewa kombe lao.

Wakati huo huo, Kocha KenGold FC Jumanne Chale ameonekana kuwa na wasiwasi na kibarua chake.

Beki huyo wa zamani wa RTC Kagera, amesema anasikia maneno maneno kuwa huenda asiendelee kuifundisha timu hiyo, badala yake ataletwa kocha mwingine.

“Huenda nisiendelee kuwa katika timu hii, au hata nikiendelea nitakuwa kocha msaidizi, lakini ndiyo soka lilivyo, nakiri kabisa kuwa hayo maneno yapo, lakini hayawezi kunifanya mimi nisiendelee kufundisha soka, mimi najua ninachofanya,” amesema kocha huyo

Ngoma awapa masharti viongozi Simba SC
Neema kuwaangukia wachimbaji wadogo