Kocha Mkuu wa Al Hilal ya Sudan Florent Ibenge ameonesha kuwa na wasiwasi, endapo watakutana na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Miamba hiyo huenda ikakutana katika Mzunguuko wa Kwanza wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika endapo itashinda michezo ya hatua ya awali.

Ibenge ambaye msimu uliopita alitwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika akiwa na RS Berkane ya Morocco, amesema kikosi cha Young Africans kina mastaa ambao amewahi kufanya nao kazi na mahiri haswa Fiston Mayele aliyeko katika kiwango bora.

“Namfahamu Fiston (Mayele) nimefanya naye kazi ni kijana wangu lakini bahati mbaya kwetu tunakwenda kukutana naye akiwa katika kiwango bora sana tutahitajika kuwa naye makini kama tukikutana,”amesema Ibenge

Katika hatua nyingine Kocha huyo amemtaja Mchezaji mwingine wa Young Africans ambaye anamuumiza kichwa Stephane Azizi Ki, ambaye aliwahi kujaribu kutaka kumsajili lakini hesabu zikagoma.

“Pia wana Azizi Ki ni mchezaji mzuri ambaye wanaweza kuwa na safu bora ya ushambuliaji, niliangalia mechi yao dhidi ya Simba nikaona jinsi wanavyohaha na Fiston.

“Niliona pia mechi hiyo wamemrudisha kucheza beki ya kati Yannick Bangala nimewahi kuwa naye na akicheza hapo anakuwa ni mtu imara zaidi, utaona jinsi walivyo na kikosi bora.”

“Tunatakiwa kujipanga sawasawa utakuwa mchezo ngumu hasa watakapokuwa nyumbani, hii ni klabu ambayo ina mashabiki wengi ambao wanaweza kujaa uwanjani, kama tukikutana nao utakuwa mchezo mgumu.”

“Kwa sasa tunaendelea kujipanga kwanza kukabiliana na St George, tunaamini hii michezo tuliocheza hapa katika haya Mashindano mafupi yatatupa ubora kwa kuwa ligi hapa bado haijaanza,” amesema kocha huyo wa zamani wa AS Vita

Young Africans itacheza michezo miwili nyumbani dhidi ya Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC, ambayo wanajipa nafasi kubwa ya kushinda na sasa hesabu zao zipo kwa Al Hilal wanaonolewa na Florent Ibenge raia wa DR Congo mwenye uzoefu na soka la Afrika.

Mieleka kuchaguana Oktoba 28
Azam FC: Tunasubiri muda ufuke