Potezea matokeo yaliyoiweka pabaya Taifa Stars kwenye mbio za kwenda Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast, mabosi wa Azam FC wamejivunia namna kituo chao cha soka la vijana kilivyochangia wachezaji kibao kwenye kikosi cha sasa cha Timu ya Taifa.
Stars ilicharazwa bao 1-0 na Uganda The Cranes katika mechi ya Kundi F iliyopigwa Jumanne Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku asilimia kubwa ya wachezaji walioitumikia timu hiyo wakiwa ni zao la Akademi ya Vijana ya Azam FC na Kocha wa timu hiyo, Kally Ongala alisema ni heshima kwa klabu yao na kwamba anaamini matunda ya kile kilichowekezwa na matajiri hao kinaendelea kulipa.
Katika kikosi cha Stars kinachoongozwa na kocha Adel Amrouche kilianza na takribani wachezaji watano walioibuliwa na kukuzwa au kuitumia Azam akiwamo Simon Msuva, kipa Aishi Manula na kiungo Mudathir Yahya ambao walipita akademi hiyo kati ya 2009-2011, Novatus Dismas aliyejiunga mwaka 2016-2020 kisha kwenda Israel na baadae kucheza Ubelgiji hadi sasa, Mohamed Hussein aliyeitumikia 2010 kisha kwenda Simba na nyota Himid Mao aliyejiunga mwaka 2008 kabla ya kutimkia Misri mwaka 2018.
Kocha Kally akilizungumzia hilo amesema kama mmoja wa makocha wa Azam aliyewanoa wachezaji hao anajivunia kuona vipaji walivyovikuza vikileta matokeo chanya sio tu kwa klabu hiyo bali hata kwa taifa.