Mabosi wa Azam FC wamebadili gia angani na kutuma ofa katika klabu ya Al Hilal juu ya kuangalia uwezekano wa kupata huduma ya Lamine Jarjou na Makabi Lolepo baada ya kuona dili la kumleta nyota wa Marumo Gallants, Ranga Chivaviro kuwa gumu.
Awali, Azam FC ilishaanza mazungumzo na meneja wa Chivaviro mwenye mabao sita kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika, lakini gazeti la Far Post la Afrika Kusini liliandika kuwa nyota huyo yupo mbioni kujiunga na Kaizer Chiefs.
Baada ya kuona mambo ni magumu na wanahitaji nguvu kwenye eneo la ushambuliaji, klabu hiyo ikaamua kutuma maombi kwa Al Hilal ya Sudan, kama inaweza kuwapata Jarjou na Lilepo kwa mkopo wa mwaka au miezi sita.
“Jarjou ni uhakika atakuja hapa, labda tu mambo yabadilike baadae, lakini upande wa Lilepo na yeye kama mambo yatabadilika kwenye upande wa fedha basi atakuwa hapa.” Chanzo Azam FC
Hata hivyo upande wa Lilepo dili linawezekana kuwa gumu kutokana na dau lake, ambalo limewekwa hata kama anatakiwa kutoka kwa mkopo ni Dola 250,000 ambazo sawa na Sh 591 milioni kwa mkopo wa mwaka.
Jambo hilo limeifanya Azam FC imgeukia upande wa Jarjou na uwezekano wa kumpata ni mkuba kutokana na mchezaji kuhitaji nafasi ya kucheza kwenye timu inayocheza mashindano ya CAF.
Sababu kubwa ya mchezaji huyo kukubali kutoka pia ni nchi ya Sudan kuwa na vita, huku ikiwa haijulikani ni lini itamalizika, wakati huo huo sehemu nyingine ligi zikiendelea.
Inaelezwa kuwa mabosi wa Azam FC tayari wameshaanza kufanya mazungumzo na Jarjou, huku wakimtumia na kocha wake mkuu, Youssouph Dabo.
Dabo ni raia wa Senegal, huku Jarjou akiwa na uraia wa Senegal na Gambia, hivyo wanazungumza lugha moja na inaelezwa kuna ushawishi mkubwa wa mchezaji huyo kutua nchini.
Chanzo kimoja kutoka ndani ya kimelidokeza kuwa Azam FC, wanataka kufanya usajili wa maana kama ilivyokuwa msimu huu, lengo ni kuongeza ushindani.
“Usajili wetu kwa kiasi kikubwa msimu huu wote wameona kwamba hatujafanya makosa makubwa kwa sababu wanacheza na wanashindana vya kutosha.
“Jarjou ni uhakika atakuja hapa labda tu mambo yabadilike lakini upande wa Lilepo na yeye kama mambo yatabadilika kwenye upande wa pesa yake basi atakuja, wote hawa ni kwa mkopo,” kilisema chanzo hicho