Kiungo Mshambuliaji kutoka Burkina Faso Stephane Aziz KI amesema anaiona Young Africans ikifunga idadi kubwa ya mabao msimu huu 2023/24, tofauti na msimu uliopita kutokana na kutokumtegemea mchezaji mmoja.

Young Africans hadi sasa ina mabao 20 kati ya hayo ni matatu tu yamefungwa na nafasi tofauti na kiungo ambapo ni bao la Dickson Job, Keneddy Musonda na Hafiz Konkoni mengine yote yamefungwa na viungo.

Aziz Ki amesema kocha Miguel Gamondi ametengeneza timu ya ushirikiano na kuhakikisha inatafuta pointi tatu muhimu bila kujali nani atafunga siku hiyo.

Young Africans ina wachezaji wengi wenye uwezo wa kuona goli hivyo kila anayepata nafasi ya kucheza anaingia uwanjani akiwa na akili ya kuipambania timu kupata matokeo mazuri apambane kufunga na kuzuia hili kwa asilimia kubwa limefanikiwa;

“Naweza nikakosa nafasi ya kufunga akafunga Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua au Clement Mzize, ukiangalia hadi mabeki wanafunga, hivyo kazi yao sio kulinda tu wanatakiwa kupanda kutengeneza mashambulizi pia wakipata nafasi wafunge kama ilivyo kwa Job,” amesema.

Aziz Ki amesema umoja walioutengeneza ndio siri kubwa ya kucheza kwa kujiamini na kutumia vizuri nafasi wanazozipata akikiri kuwa msimu uliopita haikuwa hivyo kwasababu walikuwa wanaamini katika kumtengenezea nafasi mshambuliaji tu.

Amesema Gamondi amewapa akili kubwa ambayo inawatesa wapinzani wao kila wanapokutana kwani wakimkaba yeye kwa kuamini kuwa ndiye atakayewaadhibu anafunga mchezaji mwingine ambaye hawakumtarajia.

“Hakuna raha ya kucheza mpira bila presha kutoka kwa wapinzani kama ilivyo Young Africans ya sasa tunafanya kile ambacho tunaelekezwa na kocha na kimekuwa kikitulipa ubora wetu ni kutokana na kutokujipa umuhimu tunapokuwa uwanjani kila mmoja anachukuliwa kujua anachokifanya uwanjani.” amesema kiungo huyo kinara wa upachikaji mabao.

Aziz Ki ambaye ametupia mabao sita hadi sasa kwenye mechi saba alisema malengo yao ni kutetea ubingwa na kufunga idadi kubwa ya mabao ili kujenga mwendelezo mzuri eneo hilo ambalo amekiri kuwa na mastaa wengi wenye uwezo.

Mabao 20 ya Young Africans yamefungwa na Job, Hafiz, Yao, Musonda wote bao moja moja, Pacome (3), Aziz Ki (6), Mudathir (2), Maxi Zingeli (5).

Young Africans itakutana na watani zao Simba SC, iikiwa imekusanya alama 18 sawa na Wekundu hao wa Msimbazi ambayo wapo nyuma kwa mchezo mmoja.

Mchezo huo umepangwa kuchezwa Jumapili (Novemba 05) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa 11 jioni.

Babati wachukua hatua usafi wa Mazingira, tahadhari ya El-nino
Idadi ya waliofariki kwa kimbunga yafikia 100