Uongozi wa klabu ya Aston Villa umemtangaza Dean Smith kuwa meneja mpya wa kikosi chao, na atasaidiwa na aliyekua beki wa klabu hiyo John Terry.
Smith aliyeachana na klabu ya Brentford alionyesha kuwa tayari kufanya kazi na Terry kwa kuwathibitishia viongozi wa Aston Villa, ambao walimpendekeza kabla ya kusainiwa kwa mkataba wa ajira baina ya pande hizo mbili.
Smith anakua meneja wa The Villians, baada ya kuwa shabiki wa muda mrefu wa klabu hiyo ya mjini Birmingham.
Hii inakua kama bahati kwa John Terry, baada ya kutangaza kustaafu soka mwanzoni mwa juma hili, na siku chache anathibitishiwa kuendelea kubaki klabuni hapo.
Metendaji mkuu wa Aston Villa Christian Purslow amesema: “Tunaimani kubwa na wawili hawa katika kufanikisha kazi ya kuiwezesha timu kufanya vyema katika ligi daraja la kwanza, na ikiwezekana mwishoni mwa msimu ipande daraja la kucheza ligi kuu msimu ujao.”
“Smith ametuthibitishia kuwa tayari kufanya kazi na Terry, na sisi kama uongozi tumewapa baraka zote, na tunawahakikishia kushirikina nao katika hatua zote, ili kufanikisha malengo tuliojiwekea.”
Kabla ya kutangazwa kwa Smith kama meneja, tetesi za vyombo vya habari zilizeleza kuwa, uongozi wa Aston Villa ulikua umejipanga kuingia mkataba wa aliyekuwa nahodha na mshambuliaji wa klabu ya Arsenal Thiery Henry.