Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi amewatoa hofu Watanzania kuhusu afya yake na kusema kuwa yupo vizuri na wala hasumbuliwi na maradhi yoyote.
Mwinyi ameyasema hayo jijini Dar es Salaam kuwa wakati alipokwenda kumjulia hali Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya, nyumbani kwake Upanga.
“Mimi niko vizuri nina afya njema na leo nimefanya mazoezi yangu kama kawaida kwa kutembea kilometa tano kwa mwendo wa kasi, hivyo niwatoe hofu Watanzania na wananchi kwa ujumla juu ya afya yangu,”amesema Alhaji Mwinyi.
Jana mitandao ya kijamii ilisambaza taarifa zilizodai kuwa mzee Mwinyi amefariki dunia nchini Marekani na kwamba alikwenda huko kutibiwa moyo.
Hata hivyo, Taarifa kutoka Idara ya Habari Maelezo kupitia Mkurugenzi wake ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas imekanusha taarifa hizo na kusema kuwa Mzee Mwinyi ni mzima wa afya na anaendelea na majukumu yake kama kawaida.
Dkt. Abbasi ameitaka jamii ifahamu kuwa ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mitandaoni, 2015, kwa mtu yeyote kutangaza, kuchapisha au kueneza habari za uongo au uzushi katika mitandao