Kocha wa mkuu wa Young Africans, Zlatko Krmpotic amesema kikosi chake kinahitaji angalau mwezi mmoja ili icheze kwa kiwango anachotaka huku akiwasifu wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango bora katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Aigle Noir ya Burundi.
Zlatco amesema wachezaji wake walijitahidi ingawa bado hakuna muunganiko na wataitumia siku kadhaa zilizobaki kurekebisha mapungufu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Septemba 6, ambapo watapapatuana dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam.
“Ninachowaahidi hapa kwangu ni kazi na nidhamu, huo ndio mwongozo wangu,” alisema Zlatko na kuongeza, Yanga inahitaji mazoezi zaidi ili kutengeneza muunganiko mzuri na icheze kwa ubora mkubwa.
“Si kazi rahisi kupata muunganiko wa timu kwa muda mfupi hivi, ukizingatia timu ina wachezaji 14 wapya, hivyo inahitaji muda ili kuzoeana.
“Licha ya kwamba muda ni mfupi, tutatumia wiki moja iliyobaki kuyafanyia kazi mapungufu yetu ili tuanze vizuri ligi, lakini ili timu icheze kwa ubora wake inaweza kuchukua mwezi mzima ili kuwafanya wachezaji wote kuzoeana na kucheza kwa maelewano,” amesema Zlatko.
“Nimewaangalia wachezaji wote waliosajiliwa wana vipaji vikubwa, hivyo muhimu wanatakiwa kujitoa kwa ajili ya timu na kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja,” amesema Zlatko.
Kikosi cha Young Africans jana Jumatano kiliingia kambini Kigamboni jijini Dar es salaam, kwenye majengo maarufu ya Avic yaliyojitenga na yenye utulivu mkubwa na vifaa kibao vya michezo ukiwemo uwanja wa ndani kwa ndani na hakuna mgeni anayeruhusiwa kuingia ndani bila ruhusa maalumu.
Majengo maarufu ya Avic yanamilikiwa na tajiri Kampuni ya GSM inayoidhamini Young Africans Ghalib Mohamed.