Makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu yameonesha ongezeko la asilimia 59, kutokana na mpango wa kutekeleza miradi mikubwa inayolenga maeneo manne.
Hayo yalibainika jana, Aprili Mosi, wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipowasilisha bungeni makadirio ya bajeti ya ofisi yake kwa Mwaka wa Fedha 2020/21.
Makadirio hayo yalionesha kuwa bajeti itakuwa Sh 434,588,777,000 ukilinganisha na ya Mwaka huu wa fedha ambayo ni Sh 273,069,061,181.
Alieleza miradi inayotarajiwa kutekelezwa na ofisi yake katika maeneo manne ambayo ni kuboresha huduma muhimu za kijamii kama maji, afya na elimu; kuimarisha na kurahisisha upatikanaji wa nishati; kuvutia uwekezaji zaidi na kuweka mazingira bora zaidi kwa wawekezaji; na usimamizi wenye ufanisi wa maliasili.
Hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha tunajenga Tanzania ya viwanda na kuwaletea wananchi maendeleo zaidi, kwa mujibu wa Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alisema kuwa ili kufanikisha malengo, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa kama Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa uzalishaji wa Umeme wa Mwalimu Nyerere wa MW 2,115, kuimarisha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.
Katika hatua nyingine, bajeti ya Bunge imepungua kwa asilimia mbili kutoka 124.2 bn/- ya sasa hadi 122bn/- kwa Mwaka wa Fedha 2020/21.