Serikali imepanga kuongeza kodi ya bidhaa za nywele bandia zinazotengenezwa nchini na zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuongeza mapato.
Akizungumza leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Mwaka wa Fedha 2019/2020, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa Serikali imepanga kutoza kodi ya 10% kwa nywele bandia zinazotengenezwa nchini na 25% kwa nywele bandia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
“Napendekeza kutoza kodi ya 10% kwa nywele bandia zinazotengenezwa hapa nchini na 25% kwenye nywele bandia zinazoagizwa kutoka nje ya nchi. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali,” alisema Dkt. Mpango.
Kauli hiyo iliyopata mwitikio mkubwa kutoka kwa wabunge na kusababisha Spika wa Bunge, Job Ndugai kumtaka Dkt. Mpango airudie, ilifuatiwa na mpango wa kupunguza kodi kwenye vilainishi vya ndege vinavyotengenezwa nchini na vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi.
Aidha, Dkt. Mpano alisema kuwa Serikali imepanga kuongeza bei ya kulipia leseni za udereva kutoka Sh. 40,000 hadi Sh 70,000 ikiambatana na kuongeza muda wa leseni kutoka miaka mitatu hadi miaka mitano.
Endelea kufuatilia Dar24 kupata undani wa mengi kutoka kwenye hotuba ya Dkt.Mpango akisoma Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.