Serikali ya Zanzibar, inatarajia kutumia jumla ya Shilingi 2.5 trilioni katika bajeti yake kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Akiwasilisha bajeti ya Visiwani katika Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Mipango), Zanzibar, Dkt. Saada Salum Mkuya, amesema kati ya Sh2.5 trilioni, Sh1.353 trilioni zitaelekezwa katika matumizi ya maendeleo.
Amesema, kiasi cha Shilingi 1.220 trilioni zilizobaki zitaingia kwenye matumizi ya kawaida, huku Serikali hiyo ikiwa na vipaumbele muhimu 13 katika kubadilisha taswira ya visiwa hivyo kimaendeleo.
“Kati ya Sh2.5 trilioni, Sh1.353 trilioni zitaelekezwa katika matumizi ya maendeleo na kiasi cha Shilingi 1.220 trilioni zilizobaki zitaingia kwenye matumizi ya kawaida,” amesema
Akifafanua vipaumbele hivyo, Dkt. Mkuya amesema vitakuwa ni katika maeneo ya nishati, uwekezaji, miundombinu, elimu, upatikanaji wa maji safi na salama na uchumi wa bluu.
“Maeneo mengine ya kipaumbele uwezeshaji wa umma, fedha, mawasiliano, kilimo na utalii na maendeleo ya maliasili,” alisema Dkt Mkuya.
Aidha, ameongeza kuwa katika mwaka ujao wa fedha, serikali itatumia Sh89.66 bilioni kwa shughuli zinazohusishwa na uchumi wa bluu, huku baadhi ya mambo yatakayotekelezwa yakiwa ni pamoja na ujenzi wa boti kwa matumizi ya kawaida na uvuvi wa bahari kuu.
Kiasi hicho cha matumizi ya Shilingi 2.5 trilioni, ni ongezeko la zaidi ya Shilingi 700 bilioni ikilinganishwa na Sh1.8 trilioni zilizotumika katika mwaka wa fedha wa 2021/22.