Jengo la makao makuu ya Klabu ya Young Africans lililopo makutano ya mtaa wa Jangwani na Twiga Kariakoo jijini Dar es Salaam, liko hatarini kupigwa mnada kutokana na deni la Shilingi milioni 300 ambalo klabu hiyo inadaiwa, imefahamika.
Taarifa zilizopatikana jana jijini zinaeleza kuwa Kampuni ya Udalali ya Msolopa ndiyo imepewa mamlaka ya kusimamia mnada huo.
Akizungumza jana jioni, Katibu Mkuu wa Young Africans, Boniface Mkwasa, alithibitisha kuwapo kwa deni hilo na kueleza kuwa uongozi umeanza utaratibu wa kulifanyia kazi suala hilo.
Mkwasa alisema kuwa, deni hilo limetokana na malimbikizo ya ada ya jengo la kiwanja kinachomilikiwa na klabu hiyo, lakini wanaamini watalilipa kabla ya mchakato huo wa kunadi jengo hilo la makao makuu haujafanyika.
“Ni kweli kesi ipo katika Mahakama ya Ardhi na tumeshaanza kuifanyia kazi,” alisema kwa kifupi Mkwasa, kocha na mchezaji wa zamani wa timu hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkwasa alisema, kikosi chao kipo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, ambao watapambana nao kwenye uwanja wa Taifa Dar es salaam.