Meneja wa Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Baleke ametoa ufafanuzi wa kina kuhusu tetesi za Mchezaji wake kutakiwa kurejea TP Mazembe mwishoni mwa msimu huu, baada ya kuonyesha kiwango bora wakiwa Msimbazi.
Jean Baleke alisajiliwa Simba SC wakati wa DIrisha Dogo la Usajili mapema mwezi Januari 2023, kwa mkataba wa mkopo wa muda mrefu, baada ya kukosa uhakika wa kucheza katika kikosi cha kwanza cha TP Mazembe.
Clovis Mashisha, Meneja wa Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, amesema taarifa za Baleke kutakiwa kurudi TP Mazembe ni za kweli lakini haitakuwa rahisi kwake kurejea Lubumbashi, DR Congo kama hakutakuwa na makubaliano na Uongozi wa Simba SC.
Clovis amesema Baleke anaendelea kuheshimu mkataba uliopo kati yake na Simba SC japo ni wa mkopo, na msimu ujao ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi.