Nahodha na Kiungo Mshambuliaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Wales, Gareth Bale amesema Lionel Messi atakuwa na Presha ndogo ya kushinda katika Ligi Kuu ya soka ya Marekani ‘MLS’ kwa sababu klabu za huko “zinakubali kupoteza.”

Mapema mwezi huu, Messi alitangaza kuwa ana nia ya kujiunga na klabu ya Inter Miami baada ya kuondoka Paris Saint-Germain, ingawa dili bado halijakamilika.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2022 alihusishwa na kurejea katika klabu yake ya zamani ya Barcelona lakini aliamua kuhamia Marekani na kusema alitaka kufurahia soka lake “kwa njia ya utulivu.”

Barca ilikubali uamuzi wa Messi kwa kutoa taarifa ikisema alichagua “kushindana katika ligi yenye mahitaji machache.”

Bale, ambaye alimaliza maisha yake ya uchezaji katika klabu ya LAFC, alikubali kwamba Messi angefurahia maisha rahisi nchini Marekani bila kuangaziwa mara kwa mara kushinda kila wiki. “Imepoa zaidi,” alisema Bale akiiambia BT Sport.

“Ukishindwa ukiwa Real Madrid, ni kama ulimwengu umekwisha, umesulubishwa. Unajisikia vibaya. Unarudi nyumbani na huna furaha.

“Wanakubali kupoteza zaidi (katika MLS). Hakuna matokeo. Huwezi kushuka daraja hapo hapo. Unapopoteza mchezo unakwenda kwenye mchezo unaofuata. Wanakubali kupoteza zaidi hapo.

“Wanajua jinsi ya kupoteza lakini wanasherehekea kila ushindi kama vile umeshinda ubingwa. Hakika atafu- rahia.”

Mwaka jana kabla ya kutangaza kustaafu, Bale alijiunga na LAFC kwa mkataba wa miezi 12 na kuisaidia kupata taji lao la kwanza kuu kwa kuishinda Philadelphia Union kwa mikwaju ya Penati katika fainali ya Kombe la MLS.

Mapema wiki Mmiliki wa Inter Miami, Jorge Mas aliwaambia waandishi habari kwamba klabu hiyo inapanga Messi kucheza mechi yake ya kwanza Julai 21 katika mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Cruz Azul wa Liga MX.

Wakongomani waikomalia Young Africans
Mbunge autaka urais kwa muda