Balozi wa Seychelles nchini, Maryvonne Pool, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika usimamizi wa sheria ya Afya na Usalama mahali pa mazi yenye lengo la kulinda nguvu kazi ya taifa.
Ametoa pongezi hizo leo, alipotembelea ofisi za wakala wa usalama na afya mahali pa kazi kwa lengo la kufanya usajili pamoja na kujifunza namna ambavyo taasisi ya OSHA inatekeleza majukumu yake.
Aidha, Balozi huyo ameahidi kushirikiana na OSHA katika kuviwezesha vikundi vya wakulima wadogo wanaofanya shughuli zao katika wilaya za pembezoni mwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kusajiliwa na OSHA kwa ajili ya kuendelea kupatiwa miongozo ya namna ya kujikinga na madhara yatokanayo na shughuli za kilimo.
Kwa upande wake, kaimu mtendaji mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema taasisi yake imefarijika kutambua kwamba juhudi za serikali za kulinda nguvukazi ya taifa zinaonekana.
Miongoni mwa majukumu ya OSHA, ni kusajili sehemu za kazi na kisha kuendelea kuzitembelea sehemu hizo kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kutoa ushauri wa viwango stahiki vya usalama na afya vinavyopaswa kuzingatiwa.