Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amewatembelea na kufanya mazungumzo na wanafunzi wanaosoma na kuishi mjini Wuhan nchini China.

Hii ni mara ya kwanza kwa Balozi Kairuki kuwatembelea wanafunzi hao tangu kutokea kwa mlipuko wa Uviko-19.

Katika mkutano wake na Watanzania hao, Balozi Kairuki amewasisitiza kutii sheria na maelekezo yatolewayo na mamlaka za Serikali pamoja na vyuo vyao na siku zote kukumbuka kitu kikubwa kilichowapeleka China kuwa ni kusoma na Taifa linawategemea.

Balozi Kairuki amewapongeza kwa kuwa wavumilivu na wastahimilivu katika kipindi kigumu walichopitia wakati ugonjwa wa Uviko-19 ulipoanza.
Kwa upande wao wanafunzi hao wamemshukuru Balozi Kairuki kwa kuwa nao wakati wa changamoto waliopitia.

Wakati huo huo, Balozi Kairuki pia ametembelea kampuni ya uzalishaji saruji ya Huaxin yenye makao yake makuu katika Mji wa Wuhan na kufanya mazungumzo na viongozi wa juu wa kampuni hiyo kwa malengo mapana ya kuendeleza uwekezaji wao nchini Tanzania.

Rais Ramaphosa akabidhi majukumu yake
Nabi: Manula ametunyima ushindi