Beki wa Tanzania anayecheza Ligi kuu ya Afrika Kusini, Abdi Banda amesema anaamini kwa uwezo wa Mkude anaweza kuwa dili Afrika Kusini kama atakuwa na utayari kipindi kama hiki cha mwishoni mwa msimu kwenda kupambania nafasi.
Mkude amekua kwenye matatizo ya kinidhamu dhidi ya Uongozi wa Klabu ya Simba, hali iliyopelekea kusimamishwa, na kufikishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya klabu hiyo chini ya mwenyekiti wake Seleman Kova.
Banda amesema kwa kwango cha Mkude anaona ana nafasi kubwa ya kusajiliwa kwenye moja ya klabu za Afrika Kusini, lakini inategemea na utayari wake kufanya maamuzi ya kuondoka Tanzania na kwenda kusaka changamoto mpya.
“Huwa naona kuna wachezaji wengi tena sana nyumbani Tanzania kuwa wana UWEZO wa kucheza Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL).” amesema Banda aliyewahi kucheza na Mkude Simba kabla ya kwenda Afrika Kusini kucheza klabu ya Baroka na baadaye kusajiliwa Highland.
“Kipindi kama hiki kwa Sauzi wachezaji kutoka mataifa mbalimbali wanaenda kupambania nafasi za kusajiliwa, unaweza uwa mchezaji mzuri lakini wao wakataka kukuona kama kweli au laa, niliwahi siku moja kuwa napigania namba sehemu ya kusajiliwa na mchezaji ambaye ametoka kufanya majaribio Marseille (Ufaransa).
“Tulipambana na tukabaki wawili, mimi na yeye na walikuwa wakitaka beki mmoja wa kati, jamaa aliondoka maana kuna dili lake jingine lilijipa la hela nyingi, kwa uwezo wa Mkude anaweza kufanya makubwa Sauzi kama ataamua.”
Kufuatia sakata linaloendelea kati ya Mkude na Uongozi wa klabu ya Simba, tetesi zinaeleza kuwa kiungo huyo aliecheza kwa muda mrefu kwa Mabingwa hao wa Tanzania Bara, anahusishwa na taarifa za kuondoka Msimbazi, katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu 2020/21.