Benchi la Ufundi la Kagera Sugar linaloongozwa na Kocha kutoka nchini Kenya Francis Baraza, limejinasibu kuwa tayari kwa mapambano ya kusaka alama tatu muhimu baadae leo Jumatano (Septamb 29), dhidi ya Young Africans kutoka jijini Dar es salaam.
Miamba hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara itapimana ubavu kuanzia saa kumi jioni kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera, huku Mashabiki wakitarajia kuona burudani safi kwenye mchezo huo wa mzunguuko wa kwanza msimu huu 2021/22.
Kocha Baraza amesema anatambua mchezo huo utakua na changamoto kubwa ya ushindani, lakini maandalizi aliyoyafanya kwa wachezaji wake yatakua silaha nzuri ya kupambana na kufikia lengo la kupata ushindi.
“Ni mchezo mgumu na ushindani mkubwa kwa kila timu lakini kikubwa ni kuona kwamba tunapata pointi tatu muhimu.
“Wachezaji wapo tayari na wanajua kwamba mchezo hautakuwa mgumu, mashabiki wajitokeze kuwa nasi bega kwa bega kwani mchezo wa mwanzo unahitaji kushinda ili kujenga hali ya kujiamini,” amesema.
Msimu uliopita 2020/21, Young Africans ilipocheza na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na kiungo kutoka DR Congo Tonombe Mukoko, mbaye leo ataukosa mchezo kwa kuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba SC.
Mchezo wa mzunguuko wa pili timu hizo zilipokutana Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam zilifungana mabao 3-3.