Baraza la Wawakilishi la Bunge la Marekani limewasilisha hati ya mashtaka mbele ya Baraza la Seneti dhidi ya rais wa zamani Donald Trump na kufungua njia ya kuanza kwa shauri la kihistoria kwa kiongozi wa taifa hilo kushtakiwa mara mbili na Bunge.
Wawakilishi tisa walioteuliwa kuongoza mchakato huo wamewasilisha shtaka moja pekee linalomtuhumu Trump “kuchochea uasi” baada ya wafuasi wake kuvamia majengo ya Bunge mjini Washington mapema mwezi huu.
Chuck Schumer amesema wajumbe 100 wa Baraza la Seneti ambao watafanya kazi kama mahakimu wataapishwa baadae leo na tayari wito umetumwa kwa Trump kufika mbele ya baraza hilo.
Hii ni mara ya pili kwa Trump kufunguliwa mashtaka mbele ya Bunge baada ya mwaka mmoja uliopita kushtakiwa kwa kuishinikiza Ukraine kufanya uchunguzi dhidi ya hasimu wake wa kisiasa ambaye sasa ni rais wa Marekani, Joe Biden.
Iwapo atapatikana na hatia, Baraza la Seneti linaweza kumpiga marufuku ya kushika tena madaraka, hatua itakayomzuia kuwania tena urais mwaka 2024.