Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Abdallah Mohammed ‘Bares, amesema ataingia na mfumo mwingine wa kuongeza idadi ya washambuliaji katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Geita Gold FC utakaochezwa leo Jumatatu (Agosti 21) kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Bares amesema licha ya kupata Ushindi katika mchezo wao wakwanza, ameyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza ili kuwa na kikosi imara zaidi.
Kocha huyo amesema katika mchezo wa leo ataingia tofauti ili kuwachanganya wapinzani wao na kwa sababu anafahamu mbinu za Kocha wa Geita Gold FC, Hemed Morocco, ambaye ni Mzanzibar mwenzake.
“Hii mechi yetu itakuwa ya ushindani mkubwa, naamini mbinu zitatawala zaidi katika mchezo, makocha wote tunatoka sehemu moja na kila mmoja wetu anafahamu ubora wa mwenzake.
“Utakuwa mchezo mzuri, ninategemea kufanya mabadiliko ya kikosi lakini pia kuongeza watu mbele kulingana na ubora wa wapinzani wetu katika kila eneo, tunahitaji kushinda mechi hiyo,” amesema Bares.