Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe ameendelea kutetea uamuzi wake wa kuwasilisha Bungeni hoja binafsi inayobeba mambo nane ikiwemo masuala ya utekaji, uhalifu na haki za kidemokrasia.
Mbunge huyo ambaye pia ni kada wa CCM amesema kuwa uamuzi wake ni sehemu ya kutekeleza kiapo chake kwa chama huku akidai kuwa amefanya utafiti wa kutosha wa masuala hayo tangu mwaka 2010.
“Watanzania wanalalamika na haya ninayoyafanya hapa yapo katika kiapo cha chama changu (CCM). Msingi wangu wa kubeba hii hoja ni katiba ya chama change na katiba ya nchi,” Mwananchi inamkariri Bashe.
Bashe amehoji ‘watu wasiojulikana’ akidai ni nani anayefanya matukio yote ya mauaji na utekaji ambayo yamekuwa yakiripotiwa.
Ameseha hata Rais John Magufuli amekemea matukio haya ikiwa ni pamoja na suala la kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), Akwillina Akwilline.
“Nani anafanya haya matukio, mbona hakuna haki? Rais amezungumzia mambo haya likiwemo la Akwillina. Ila kauli ya Rais haizuii kufanya haya niyafanyayo,” Bashe anakaririwa.
Aidha, Bashe aliongeza kuwa katika kikao cha Bunge litakalojadili hoja zake, ataheshimu mawazo ya wabunge wote watakaochangia.