Matokeo ya sare ya bila kufungana yaliyopatikana kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kati ya Atletico Madrid dhidi ya Bayer Leverkusen yalitosha kuwavusha The Mattressers.
Atletico Madrid ambao walikua nyumbani usiku wa kuamkia leo, waliingia uwanjani huku wakiwa na faida ya ushindi wa mabao manne kwa mawili walioupata kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza, uliounguruma nchini Ujerumani majuma mawili yaliyopita.
Hata hivyo haikuwa kazi rahisi kwa Atletico Madrid kutimiza lengo la kufaulu mtihani wa kutinga katika hatua ya robo fainali, kutokana na wapinznai wao kuonyesha soka la ushindini, lakini umahiri wa mlinda mlango Jan Oblak ulisaidia kuokoa michomo miwili iliyoelekezwa langoni kupitia kwa Julian Brandt na Kevin Volland.
Hali kadhalika kwa upande wa mlinda mlango wa Bayer Leverkusen Bernd Leno alionyesha ujuzi wa kupangua mashuti ya Angel Correa na Koke.
Ushindi wa jumla wa mabao manne kwa mawili, unaifanya Atletico Madrid kuungana na klabu nyingine saba zilizotinga hatua ya robo fainali, ambazo ni AS Monaco, Bayern Munich, Borussia Dortmund, Leicester City, Juventus, FC Barcelona na Real Madrid.