Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini, ambazo zimeanza kutumika hii leo Jumatano, Tarehe 3 Agosti 2022.
Bei hizo za mafuta zimezidi kupaa ambapo imepanda kwa Shilingi 190 kwa kila lita ya mafuta ya Petroli lita na Shilingi 179 kwa kila lita ya mafuta ya Dizeli na mafuta ya taa yakipanda kwa Shilingi 323 kwa kila lita kwa Jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), imesema bei ya rejareja kwa jiji la Dar es Salaam itakuwa Shilingi 3,410 kwa lita moja ya Petroli na Shilingi 3,322 kwa dizeli na mafuta ya taa yakifikia Shilingi 3,765.
Bei hii mpya ambayo imeanza kutumika leo Agosti 3, 2022 kwa mwezi uliopita Petroli ilikuwa ikiuzwa Shilingi 3,220, lita ya Dizeli mwezi uliopita iliuzwa kwa Shilingi 3,143 na mafuta ya taa yalikuwa yakiuzwa kwa Shilingi 3,442.
Ewura imesema bei hizo mpya zinatokana na bei za Mafuta katika soko la dunia kuongezeka na kusababisha bei za mafuta katika soko la ndani kuongezeka pia na kwamba zimejumuisha ruzuku ya Shilingi 100 bilioni iliyotolewa na Serikali.
EWURA imesema “Tunapenda kuukumbusha umma kwamba bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kwa eneo husika zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba 15200# na kisha kufuata maelekezo. Huduma hii ni bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini.”
Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya Petroli zitaendelea kupangwa na soko na EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta.
Endapo Serikali isingetoa ruzuku hiyo, lita ya Petroli ingeuzwa Shilingi 3,630 na Dizeli Shilingi 3,734 kwa jijini Dar es Salaam, na ili kupunguza madhara ya ongezeko hilo katika soko la ndani, Serikali imetoa ruzuku ya bilioni 100 kwa ajili ya bei za mafuta hapa nchini kwa Agosti 2022.