Kampuni ya Kopafasta, imeanzisha programu yake ya mafuta kadi inayolenga kuwasaidia madereva wa vyombo vya moto, kujikwamua na tatizo la kuishiwa mafuta wawapo katika majukumu yao, ikiwahusisha pia Watanzania wote wenye uhitaji wa huduma hiyo.

Mpango huo wa mafuta kadi, unafanyika kwa kuvihusisha vituo vya mafuta vilivyoainishwa kutoa huduma hiyo, ambapo mteja atapatiwa kadi rasmi ya kumuwezesha kujaza kiasi cha mafuta na kisha kulipa baadaye kila mwezi.

Akiiongelea huduma hiyo, Mkurugenzi wa Kopafasta, Patrick Kang’ombe amesema mafuta kadi itasaidia kuweka nidhamu ya utumumiaji wa mafuta kwa wahusika wenye vyombo vya moto na kwa kupunguza safari zisizo za lazima kitu kitakachowafanya kujiongezea kiwango cha uwekaji wa akiba binafsi.

Dereva wa Pikipiki akiwa katika kituo cha mafuta akishikilia bango la Mafuta kadi na Muhudumu wa Kituo cha mafuta mara baada ya kupatiwa Huduma.

“Ni rashisi sana kujiunga na huduma hii, na ili kuondoa mkanganyiko mteja afike ofisini kwenu Garden Street, Mikocheni Dar es Salaam ili kupata maelekezo ya kina na kujipatia mafuta kadi itakayomuwezesha kutamba mjini,” amefafanua Kang’ombe.

Amesema, “kopafasta kama skimu, ilianzishwa kwa madhumuni ya kujumuisha kifedha na kurasimisha vikundi kutoka sekta zisizo rasmi na zisizotambuliwa, ambazo huchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Taifa.”

Aidha, Mkurugenzi Patrick ameongeza kuwa, bidhaa na huduma za kopafasta zimeundwa ili kuinua vikundi baada ya kusajiliwa, kutambuliwa na kudhibitiwa kupitia miradi ya Serikali kama vile TACIP na PSG-P ambapo mikopo ya yake inapatikana kupitia maombi ya mtandaoni kwa kutumia simu janja na huduma za pesa za kielektroniki.

“TACIP ni Mradi wa Utambulisho wa Sanaa na Ufundi Tanzania na PSG-P ni Mradi wa Walinzi wa Kibinafsi, na kufanya kopafasta kuwa na kauli mbiu isemayo “Microfinance with the difference” kutokana na kuhusiana kwa ajenda ya Serikali,” amesema.

Ameongeza kuwa, ajenda hizo ni pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi kwa kutoa mikopo ya fedha taslimu ili kuwainua wanachama kwa kuwapatia mitaji na mikopo ya vifaa na kuweza kufanya uzalishaji, kutokana na kukua kwa uzalishaji wa sekta rasmi unaongeza wigo wa kodi na kuliongezea Taifa mapato.

“Pia ajenda nyingine ya Kopafasta ni kukuza msingi wa viwanda kwa kutoa mikopo ya kodi kwa wazalishaji wadogo ikiwemo useremala, jambo litakalosaidia kuongeza amani na utulivu nchini, vilevile tunatoa mikopo kwa walinzi wa makampuni binafsi mpango ambao pia utasaidia kupunguza uhalifu,” amesisitiza Partick.

Uzinduzi wa programu hiyo ya mafuta kadi, unaendana na kauli mbiu isemayo “jaza mafuta lipa baadaye” na kufanya watu wengi kuielewa program hii ambayo inawafanya wahitaji kuwa na shauku kubwa ya kuwa na kadi hiyo ambapo kwasasa, huduma hiyo ya mafuta kadi ya kopafasta inapatikana nchi nzima.

Kopafasta, inalenga kuboresha maisha ya watu wa sekta mbalimbali za uzalishaji mdogo, kwa kutoa huduma zake kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu, kupitia mtaji wa kitaalamu na wa kujitolea huku ikiwakaribisha wamiliki wote wa vyombo vya moto wakiwemo madereva wa bajaji na pikipiki, kujiunga na mpango wa mafuta kadi.

Jeshi laanzisha msako mauaji watu 32
Nusu ya watoto wenye UKIMWI hawapatiwi matibabu