Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), limetangaza kushuka kwa bei za vyakula kwa mwezi Julai, 2022 na kuashiria kushuka kwa mwezi wa nne mfululizo tangu zilipoweka rekodi ya juu zaidi mwanzoni mwa mwaka kufuatia vita ya Ukraine.
Taarifa ya FAO iliyotolewa Agosti 5, 2022 jijini Rome Italia imesema bei ya chakula inayokuwa ikisubiriwa kwa kuangalia bei za kimataifa za bidhaa tano za vyakula ambazo ni nafaka, mafuta ya kupikia, bidhaa za maziwa, nyama na sukari ilikuwa na wastani wa pointi 140.9 mwezi Julai sawa na pointi 8.6 chini ikilinganishwa na mwezi Juni.
Mchumi Mkuu wa FAO, Maximo Torero amesema kupungua huko kumetokana na kushuka kwa asilimia mbili kwa bei ya mafuta yakupikia na nafaka, huku makubaliano ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu mauzo ya nafaka za Ukraine yakichangia punguzo hilo.
Amesema, “Hata hivyo, kutokuwa na uhakika kumeendelea kusalia, kama bei ya juu ya mbolea ambayo inaweza kuathiri matarajio ya uzalishaji wa siku zijazo wa wakulima, hali mbaya ya kiuchumi ya kimataifa, na mienendo ya thamani ya fedha kuyumba kunaleta matatizo kwa uhakika wa chakula Duniani.”
Julai 2022, Fahirisi bei ya mboga ya FAO ilipungua kwa asilimia 19.2 ikilinganishwa na mwezi Juni na ikiashiria kiwango cha chini kwa miezi 10 huku nukuu za kimataifa za aina zote za mafuta zikishuka na bei ya mafuta ya mawese ikipungua kutokana kwa nchi wazalishaji.
Bei ya mafuta ya alizeti pia ilishuka kutokana na kupungua kwa mahitaji ya uagizaji bidhaa duniani, licha ya kutokuwa na uhakika usafirishaji katika eneo la Bahari Nyeusi huku thamani za mafuta ya yakupikia pia zikipungua.