Serikali imesema, inatambua mchango wa wahandisi wanawake nchini hivyo wajiandae kwa fursa na ajira mbalimbali zitakazotokana na miundombinu inayojengwa kwa wingi nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Saba la Wahandisi Wanawake Tanzania (TAWECE), lililoandaliwa na Taasisi ya Wahandisi Tanzania – Kitengo cha Wanawake na kudhaminiwa na Kampuni ya AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited, kama mdhamini mkuu.

Majaliwa amesema, hadi sasa Tanzania ina jumla ya wahandisi 30,921 wanawake wakiwa ni 3,912 sawa na asilimia 12, na kwamba Serikali imefanya uamuzi wa kujenga shule za ufundi wa kisayansi za wanawake katika kila mkoa, ili kuongeza idadi yao katika tasnia ya uhandisi.

“Wanawake mnaweza na wanawake wahandisi mnaweza zaidi, nilipata fursa ya kutembelea Daraja la Tanzanite, ambapo mhandisi aliyetoa maelezo mwanzo mpaka mwisho alikuwa mwanamke, mji wa Serikali Dodoma mhandisi anayesimamia ujenzi wa mradi huo unaoendeshwa na TBA ni mwanamke, mifano ipo mingi,” amesema Waziri Mkuu.

Awali, akizungumza katika kongamano hilo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alisema uhandisi kwa wanawake utaongezeka na kuimarika iwapo wataendelea kushirikiana kuwahamasisha wenngine kujiunga na fani hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kitengo cha wahandisi wanawake Tanzania, Mhandisi Upendo Haule alisema wanawake ni viongozi mahiri na makini wakipewa fursa na kwamba wanaiomba Serikali iendelee kuwapa fursa ili waendelee kuliwakilisha vyema taifa la Tanzania.

Wakiongea katika kongamano hilo, baadhi ya washiriki akiwemo Mhandisi wa mifumo ya kampuni ya AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited, Zuhura Khamis amesema ni jambo la furaha kukutana na wahandisi wanawake wengi wenye vipaji ili kupata utatuzi wa changamoto mbalimbali na msukumo wa kikazi kutoka kwa wabobezi wa taaluma hiyo.

Katika kongamano hilo, Waziri Mkuu Majaliwa pia alikabidhi cheti cha shukrani kwa Makamu wa Rais wa Kampuni ya AngloGold Ashanti – Geita Gold Mining Limited, Simon Shayo, na kuipongeza Kampuni hiyo kwa kwa juhudi zake za kuwezesha ustawi wa wahandisi wanawake nchini Tanzania.

Rais aridhia kutolewa fedha miradi ya Wananchi
Bei za vyakula soko la Dunia zashuka