Mabosi wa Azam FC wanaripotiwa kuwa katika mawindo makali ya kusaka Saini ya beki wa kushoto wa timu ya Taifa ya Senegal na klabu ya Teungueth, Cheikh Sidibe mwenye umri wa miaka 24, ili kuziba pengo la Bruce Kangwa ambaye huenda akaachwa baada ya mchezo wa leo Jumatatu (Juni 12) wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Awali, iliripotiwa kuwepo kwa mvutano wa uamuzi kwa viongozi wa timu hiyo juu ya mustakabali wa Kangwa mwenye umri wa miaka 34 ambaye umri unaonekana kutumpa mkono. Upo upande ambao unataka aendelee kuwa kikosini huku mwingine ukitaka aondoke.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, kati ya majina ambayo yapo mezani na yanatazamwa kama mbadala sahihi wa Mzimbabwe huyo ni Sidine ambaye katika fainali za CHAN pale Algeria alifanya vizuri na kuwaongoza Senegal kutwaa taji kisha kuingia kikosi bora cha michuano hiyo.
Kushindwa kwa wachezaji wa ndani kufua dafu mbele ya Kangwa, kumewafanya Azam FC kufanya mazungumzo na Msenegal huyo na tayari ameonyesha nia ya kujiunga na matajiri hao ambao siku chache zilizopita walimtambulisha, Feisal Salum kuwa sehemu ya kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao.
Mmoja wa viongozi wa Azam FC amethibitishia uwapo wa dili hilo kutokana na timu hiyo kuwa na mpango wa kuachana na Kangwa, “Ambacho watu hawajui ni kwamba tajiri (Yusuf Bakhresa) anataka kuona timu ikifanya vizuri kuanzia kwenye ligi ya ndani hadi Afrika.”