Beki wa US Monastir ya Tunisia Ousmane Adama Ouattara amesema, wapo tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa kwanza Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Tanzania Young Africans.

Miamba hiyo itakutana Februari 12 mjini Tunis-Tunisia, katika mchezo wa Kundi B, huku kila upande ukihitaji kuanza vizuri hatua hiyo, kwa kuokota alama tatu muhimu.

Ouattara, ambaye aliwahi kucheza AS Vita 2019-2021, amesema wanatambua Young Africans ni timu nzuri na ina Mshambuliaji hatari Fiston Mayele, hivyo wanapaswa kuwa makini wakati wote wa mchezo huo.

“Mayele ni Mshambuliaji hatari, ninamfahamu vizuri kwa hiyo inatupaswa kuwa makini sana wakati wote wa mchezo, kutokana na uwezo wake.”

“Mayele ni Mshambuliaji wa Kati lakini ana Spidi kubwa sana, nafahamu kuna wachezaji wengi Young Africans na ni wazuri, lakini kwa Mayele tunapaswa kuwa makini sana.”

“Nimewahi kucheza na Mayele, ninamfahamu vizuri sana na baadhi ya mbinu zake ninazifahamu, lakini yote haya itakua kazi bure kama tutashindwa kuwa naye makini wakati wote.” amesema Ouattara

Ousmane Adama Ouattara

Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es salaam kuelekea Tunis-Tunisia, baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC utakaopigwa Kesho Jumamosi (Februari 04), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Rais wa Klabu hiyo Injinia Hersi Said amesema: “Maandalizi yote yamekamilika kwa kiasi kikubwa, mchezo wetu unatarajiwa kuwa Februari 12 mwaka huu, hivyo tunajiandaa kuhakikisha kikosi kinasafiri mara tu baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC (Jumamosi hii).”

Baada ya mchezo dhidi ya US Monastir, Young Africans itarejea nyumbani Dar es salaam kucheza dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo Februari 19, kisha itakwenda nchini Mali kuikabili Real Bamako, katika Uwanja wa du 26 Mars, mjini Bamako Februari 26.

Machi 08, Young Africans itacheza Mchezo wa Mzunguuko wa Nne wa Kundi D dhidi ya Real Bamako Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Kabla ya kuikaribisha US Monastir Machi 19. Wananchi watamalizia ugenini kwa kukabili TP Mazembe mjini Lubumbashi katika Uwanja wa TP Mazembe, April 02.

Moses Phiri aitaka Horoya AC
Lissu: Siuwazi urais wa Tanzania