Siku nne kabla ya Simba SC kucheza mchezo wa mwisho wa kutafuta tiketi ya kufuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Kocha Mkuu wa Wekundu hao Abdelhak Benchikha, amesema ana matumaini ya kikosi chake kufuzu hatua itakayofuata.

Simba SC itaikaribisha Jwaneng Galaxy ya Botswana, katika mchezo wa Mzunguuko wa sita wa Kundi B, utakaopigwa Ijumaa (Machi 2), katika Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Kikosi cha Simba SC kitaikaribisha Jwaneng Galaxy huku kikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa suluhu na Asec Mimosas zilipoumana Ijumaa (Februari 23) mjini Abidjan-Ivory Coast, hivyo kitahitaji ushindi ili kujisafishia njia ya kutinga Robo Fainali.

Benchika amesema pamoja na kubakiwa na mchezo mmoja, kikosi chake kina uhakika wa kufanya vizuri na ataanza kukiandaa haraka kwa lengo la kujiweka tayari huku akisisitiza Simba SC ina nafasi ya kusonga mbele.

Kocha huyo kutoka nchini Algeria amesema timu itarudi ikiwa na nguvu ya kuanza na maandalizi ya kuwavaa wapinzani wao na kutafuta alama za kufuzu hatua inayofuata.

“Tunajiandaa kuikabili Jwaneng Galaxy ambayo nayo inataka matokeo mazuri, kwa kuwa tutakuwa nyumbani tutahakikisha tunapambana kwa nguvu zote na kupata ushindi,” amesisitiza Benchika.

Katika msimamo wa Kundi B, Simba SC inashika nafasi ya pili ikiwa na alama sita sawa na Wydad Casablanca iliyopo nafasi ya tatu huku Asec Memosas ikiwa tayari imefuzu Robo Fainali baada ya kuongoza kundi ikiwa na alama 11 na Jwaneng Galaxy inashika nafasi ya mwisho ikiwa na alama nne.

Timu hiyo ilianza mechi za Kundi B kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Asec Mimosas ikatoka suluhu na Jwaneng Galaxy, ikafunga bao 1-0 dhidi ya Wydad Casablanca, ikaichapa mabao 2-0 Wydad Casablanca kabla ya Ijumaa (Februari 23) kutoka suluhu na Asec Mimosas ugenini Abidjan.

Benzema amaliza utata mitandaoni
Gamondi- Haikuwa rahisi kihivyo