Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, raia wa Algeria ambaye alitua na msaidizi wake Farid Zemiti na kocha wa viungo Kamal Boudjenane amempa mzawa, Seleman Matola jukumu la kupendekeza na kusajili wachezaji wazawa kwenye dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa rasmi juma lijalo.
Matola ambaye ana mkataba wa kuifundisha timu ya vijana ya Simba alirudishwa timu kubwa baada ya kuondolewa kwa kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ hivyo uongozi wa Simba SC ulimpa nafasi hiyo kocha huyo mzaiwa kwa kusaidina na Daniel Cadena kukaimu hadi walipompata kocha mpya.
Habari zinaeleza kuwa Benchikha ameridhia kumpa jukumu hilo Matola ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba SC, kwani anawajua vizuri wachezaji wa ndani zaidi yake na Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, pia imebariki suala hilo.
Chanzo cha kuaminika kutoka Simba SC kimesema kwenye usajili huo, Matola atashirikiana na Cadena kuandaa ripoti nzima ya kikosi chao na kutoa mapendekezo ya nani abaki na nani waachane nao katika kipindi hiki cha usajili wa Dirisha Dogo unaofunguliwa rasmi Desemba l6, mwaka huu.
Imefahamika kuwa baada ya usajili kukamilika basi uwepo wa Matola kwenye kikosi hicho utaamuliwa na Benchikha ambaye kama ataendelea kumuhitaji atabaki lakini kama ataona imetosha basi Matola atarudi kwenye majukumu yake ya timu za vijana.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah Try Again’ aliwahi kusema kuwa Kocha Mkuu na Benchi lake ndio watahusika zaidi katika usajili ujao na uongozi uko tayari kufanya matumizi makubwa ingawa wanaamini hawawezi kupata mastaa wakubwa kutokana na muda kuwa mfupi.
“Usajili tutafanya kadri kocha mkuu na benchi lake watakavyotaka. Tupo tayari kuwapa ushirikiano kwa asilimia l00,” alisema Try Again ambaye ni mzoefu kwenye soka la Afrika tangu enzi za Friends of Simba ambalo ni kundi lililokuwa likiendesha mambo mengine klabuni hapo.
Wekundu hao huenda wakafumua asilimia kubwa ya kikosi chao kwenye dirisha hili kwani Benchikha ameonekana kutovutiwa na viwango vya baadhi ya wakongwe ambao wengi ameanza kuwatoa kwenye program zake na viongozi wameanza kumalizana nao kimyakimya.
Simba SC iliwasili Dar es salaam jana Jumatatu (Desemba 11) ikitokea Morocco ilikopoteza mchezo wa mzunguuko watatu wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ikifungwa 1-0 na Wydad Casablanca katika dakika za nyongeza na leo itaanza maandalizi ya mechi ijayo ya ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Kagera Sugar itakayopigwa ljumaa hi Desemba 15, kwenye uwanja wenye nyasi bandia wa Uhuru, jijini Dar es salaam.