Benki kuu ya Tanzania (BOT), imesema imebaini uwepo wa baadhi ya kampuni na watu binafsi wanaojihusisha na biashara ya kutoa mikopo bila ya kuwa na leseni jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Kupitia taarifa yake iliyotolewa hii leo Novemba 24, 2022 na Ofisi ya Gavana BOT imesema inapenda kuutarifu umma kuwa taasisi, kampuni na mtu binafsi wasio na leseni husika hawaruhusiwi kufanya biashara ya kukopesha.
Aidha, taarifa hiyo imezidi kufafanua kuwa kwa atakayekiuka kifungu cha 16(2)(a) cha sheria ya huduma ndogo za fedha ya mwaka 2018 atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na faini isiyopungua shilingi milioni 20 au kifungo cha miaka miwili.
Hata hivyo, BOT pia imewaasa wananchi kuepuka kukopa au kufanya bviashara na taasisi, kampuni au mtu binafsi ambaye hana leseni za biashara ya kukopesha zilizotolewa na Benki kuu ya Tanzania.