Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ ametoa pole kwa Wanachama na Mashabiki wa Klabu hiyo, kufuatia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City.

Simba SC ilipata matokeo hayo jana Jumatano (Novemba 23) ikicheza ugenini Jijini Mbeya katika Uwanja wa Kumbukumbu ya sokoine, ikitangulia kufunga kwa bao la Mzamiru Yassin Kipindi cha Kwanza, lakini Mbeya City ilisawazisha kupitia kwa Tariq Seif Kiakala Kipindi cha Pili.

‘Try Again’ amewasilisha salamu hizo za pole kupitia Akaunti yake ya Mtandao wa Instagram akiandika: “Poleni Wanasimba wote. Tuna kazi ya kufanya mbele yetu.”

Simba SC imepoteza mchezo mmoja moja dhidi ya Azam FC (1-0), huku ikiambulia sare nne dhidi ya Young Africans, KMC FC, Singida Big Stars na Mbeya City.

Kwa mazingira hayo Simba SC inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 28, ikitanguliwa na Azam FC yenye alama 29 sawa na Young Africans iliyo kileleni.

Young Africans bado ina michezo miwili mkononi, ikitarajiwa kushuka Dimbani Jumamosi (Novemba 26) kucheza dhidi ya Mbeya City katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Benki kuu yaonya kampuni za mikopo
Majaliwa ataka mkakati maeneo ya uwekezaji SGR