Benki Kuu ya Kenya (CBK) imeziadhibu benki tano kubwa nchini humo baada ya kubainika kuwa zilihifadhi zaidi ya $35milioni zilizoibwa kutoka kwenye mfuko wa National Youth Service (NYS).
CBK imeeleza wiki hii kuwa imekamilisha sehemu ya kwanza ya uchunguzi wake kuhusu benki zilizotumiwa na watu ambao walichota fedha za NYS na kuzihifadhi kinyume cha sheria.
“Uchunguzi wetu ulitoa kipaumbele kwa mabenki ambayo yanatunza kiasi kikubwa cha fedha ambayo ni pamoja na Standard Chartered Bank Kenya Ltd, KCB Bank Kenya Ltd, Co-oporative Bank of Kenya Ltd na Diamond Trust Bank Kenya Ltd,” imeeleza taarifa ya Benki Kuu.
Imeongeza kuwa uchunguzi huo umeonesha kuwa viongozi wa benki hizo ulikiuka sheria ya kudhibiti utakatishaji fedha na kuzuia ufadhili wa kifedha kwa makundi ya kigaidi kwa kushindwa kutoa taarifa kuhusu kiasi kikubwa cha fedha zilizochotwa kama fedha taslim na kutowahoji wateja waliochukua kiasi hicho.
Pia, CBK imesema kuwa kwa mujibu wa sheria hizo, viongozi wa benki hizo walipaswa kutoa taarifa Benki Kuu endapo wangeona kuna hali ya kutatanisha kuhusu uchukuaji wa fedha taslim kwa kiwango kikubwa kwenye benki zao uliofanywa na watu binafsi, lakini hawakufanya hivyo.
Kutokana na hali hiyo, CBK imeshusha rungu la faini ambapo KCB Group wanatakiwa kulipa $1.5 milioni, Equity Bank $895,000, Standard Chartered $775,000, Diamond Trust Bank $560,000 na Co-Operate Bank $200,000.
Aidha, Benki Kuu imesema kuwa uchunguzi wa awamu ya pili unaendelea na kwamba unafanywa na taasisi nyingine kwa maelekezo ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai.