Benki ya Dunia imeahidi kutoa fedha zaidi kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini- TASAF, unaofadhiliwa na Benki hiyo kwa kushirikiana na Tanzania kwa kuwa awamu ya kwanza na ya pili ya mpango huo umeonyesha matokeo chanya kwa kuboresha maisha ya Watanzania kiuchumi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia nchi 22 zilizopo Kanda ya Afrika, Anne Kabagambe, wakati alipofanya ziara ya kuangalia utekelezaji wa TASAF awamu ya kwanza na ya Pili katika Mtaa wa Keko Machungwa Kata ya Miburani, Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa ameshuhudia mwenyewe wanawake wakiwa wamezalisha bidhaa mbalimbali vikiwemo viatu, vikapu, shanga, mikoba, vyungu, urembo na nguo zilizotengenezwa kupitia mpango wa TASAF, jambo linalodhihirisha manufaa ya mpango huo kwa Kaya masikini katika kukuza uchumi wao.
“Kwa kuwa nawakilisha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania katika Benki ya Dunia, Washington Marekani, nimejionea kwa macho yangu bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa hasa na wanawake, hivyo naenda kupeleka ujumbe huo muhimu ili Benki iweze kuongeza fedha zaidi kwa awamu zingine kwa ajili ya mpango huu wa TASAF kutokana na manufaa yake katika kupunguza umasikini nchini Tanzania,”amesema Kabagambe.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Keko Machungwa, Uwessu Misanga, amesema kuwa kuanzia mwaka 2015 hadi Februari, 2019, fedha walizolipwa walengwa wa Kunusuru Kaya Masikini katika eneo lake ni takribani Sh. milioni 86.1.
Misanga ameyataja mafanikio waliyoyapata kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kipato kwa walengwa kutokana na biashara ndogo ndogo zinazofanywa na kaya hizo lakini pia kuboreshwa kwa mahitaji muhimu ya wanafunzi kutokana na ruzuku.
Pia amebainisha kuwa changamoto za utekelezaji wa Mpango wa TASAF kuwa ni pamoja na ukosefu wa elimu ya ujasiriamali, baadhi ya Kaya kukosa fursa ya kuingia kwenye mpango, uhaba wa maeneo ya kufanyia shughuli za kuongeza kipato na pia uhaba wa mitaji katika vikundi vya wajasiriamali vilivyoanzishwa na Kaya hizo.
Baadhi ya wanufaika wa TASAF waliotoa shuhuda zao mbele ya Mkurugenzi huyo wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Anne Kabagambe, wameishukuru Benki ya Dunia kwa kuwawezesha kujikwamua kimaisha na pia wameomba kuendelezwa kwa mpango huo kwa kuwahusisha watu wengi zaidi na kuwatafutia masoko ya bidhaa zao.