Beyonce Knowles, mrembo mwenye umbo na sura yenye mvuto aliyejaliwa sauti ya ndege tetere iliyoyakuna maskio ya dunia alijikuta akiivaa aibu baada ya kupigwa kofi kali akiwa katikati ya umati tena wakati wimbo wake mpya ukichezwa.
Mwaka 2000, mwimbaji huyo, akiwa na umri wa miaka 19 alikuwa mmoja wa wanafamilia wa Destiny’s Child. Wakati huo ndio anaanza kuupata umaarufu ulioanza kumlevya taratibu. Hivyo, alijikuta tu amejisahau na kumletea mapozi na mikogo mama yake mzazi Tina, wakiwa ndani ya duka kubwa (supermarket).
Mama akaona ‘haka katoto kanaanza kunipanda kichwani kisa umaarufu, ngoja nikakumbushe asili yetu kuwa mimi ni mama yake tena wa Kiafrika na huwa hatukubali ujinga’. Akamzaba kibao kile cha kushikisha adabu, watu wote wakaanza kumuangalia na bahati mbaya kulikuwa na wanaume wale matozi ambao Bey anasema alikuwa anawaonesha mapozi kwa sababu walikuwa wameshamjua.
Beyonce ambaye hivi sasa ni mama wa watoto watatu na mke wa bilionea, Jay Z hataisahau siku hiyo. Alisimulia kilichomkuta alipozungumza na Jarida la Daily Telegraph la Uingereza.
“Tulikuwa kwenye duka kubwa, mama na baba [Mzee Mathew ambaye alikuwa meneja wangu pia] walikuwepo na wimbo wangu ulikuwa unapigwa wakati tunafanya manunuzi, nilianza kuvimba kichwa,”
“Mama alikuwa ananiuliza kitu na nikaanza kuimba [nafuatisha wimbo wangu uliokuwa unachezwa]. Na kulikuwa na wanaume wazuri sana mle ndani ambao walikuwa wananiangalia kwa jicho fulani, walinitambua. Sasa, mama yangu alianza kuniongelesha. Na mimi nikaendelea tu kujiimbisha… alinipiga kibao kizito usoni, kizito sana,” Beyonce alisimulia.
“Baba yangu akashtuka, akauliza, ‘unafanya nini’. Kwa sababu sikuwahi kupigwa kibao tangu nimezaliwa. Hawakuwa wanaamini katika hilo. Mama alijibu ‘anadhani ni supa staa kwa sababu wimbo wake umetoka. Hakuna anayejali kuhusu hilo. Wewe bado ni mwanangu. Nilikuleta kwenye hii dunia; ninaweza kukuondoa kwenye hii dunia! Sasa, kakae kwenye gari’,” alisimulia.
Hata hivyo, Beyonce anaeleza kuwa maumivu yale ya kofi zito mbele ya umati ndiyo yaliyomsaidia kwa sababu aligundua kuwa alikuwa anaanza kupoteza muelekeo kwa kulewa umaarufu mdogo alioanza kuupata.
Miaka miwili baadaye, Beyonce aliacha albam yake ya kwanza ‘Dangerously in Love. Albam hiyo ilipata mafanikio makubwa dunia nzima, ilishika nafasi ya kwanza kwenye Billboard 200 nchini Marekani.
Hii ni Alhamisi ya Kumbukizi (Throwback Thursday) kupitia Dar24. Endelea kutufuatilia tukujuze yaliyowahi kutokea, usiyoyajua na unayoyajua tukujuze kiundani.