Uongozi wa Klabu Biashara United Mara umewaomba wadau wa klabu hiyo kujitoa kwa hali na mali ili kuhakikisha timu yao inabaki Ligi Kuu kwa msimu ujao wa 2022/23.

Biashara United Mara imekua na wakati mgumu msimu huu, hali ambayo inatia hofu ya kushuka daraja huku michezo minne ikisalia, kabla ya msimu huu 2021/22 kufikia ukingoni.

Uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake Makuu mjini Musoma mkoani Mara umekiri kuwa, wanawachezaji wazuri ila nafasi waliyopo sio rafiki hadi sasa, hivyo wanawaomba wadau wa klabu hiyo kuwasapoti.

“Bado tuna nafasi ya kubaki Ligi Kuu, licha ya kuwa na matokeo mabaya kwa siku za karibuni, Wadau wetu tunawaomba wajitoe kwa hali na ali ili kuinusuru timu yetu isishuke daraja msimu huu.” imeeleza taarifa ya klabu hiyo

Katika kuhakikisha timu hiyo inabaki Ligi Kuu Biashara United Mara imejizatiti kukusanya alama 10 kati ya 12 kwenye michezo yao iiyosalia msimu.

Biashara United Mara hadi sasa ina michezo minne dhidi ya Kagera Sugar (Ugenini), Geita Gold (Ugenini), KMC FC (Nyumbani) na Azam FC (Ugenini).

Hadi sasa Biashara United Mara ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa alama 24, baada ya michezo 26.

14 hatarini kutemwa Young Africans
Juliano Belletti aipa mbinu Taifa Stars