Klabu ya Biashara United Mara imeungana na Mbeya Kwanza FC katika safari ya kushuka daraja msimu huu 2021/22, baada ya kupoteza mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC iliyokua nyumbani Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.
Biashara United Mara iliyohitaji ushindi katika mchezo huo, huku ikiiombea Tanzania Prisons kupoteza dhidi ya Ruvu Shooting, imeshindwa kufanya hivyo na kujikuta ikiambulia kichapo cha 4-1.
Matokeo hayo yameifanya klabu hiyo kubaki na alama 28 ambazo hazitoshi kuibakiza katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu kwa msimu ujao wa 2022/23.
Tanzania Prisons nayo imepoteza dhidi ya Ruvu Shooting kwa 1-0, hivyo itacheza mchezo wa mtoano (Play Off), dhidi ya JKT Tanzania inayowania kucheza Ligi Kuu msimu ujao, ikitokea Ligi daraja la Kwanza.
Tanzania Prisons imeendelea kuwa na alama 29, ikitanguliwa na Mtibwa Sugar ambayo pia imepoteza dhidi ya Young Africans kwa kufungwa 1-0, hivyo imeendelea kubaki na alama 31 zinazoiweka nafasi ya 13.