Joe Biden amefungua kinyang’anyiro cha Jumanne Maalum na ushindi katika majimbo saba, na kuiendeleza kasi ambayo imeifufua haraka kampeni yake ya kuwania uchaguzi wa rais nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic.
Seneta Bernie Sanders amenyakua ushindi katika jimbo la nyumbani Vermont, na Colorado, wakati Biden akibeba Minesota, Alabama, Tennessee, Oklahoma, Arkansas na majimbo muhimu ya North Carolina na Virginia.
Kwamujibu wa DW vituo vya kupiga kura vimefungwa katika majimbo mengi kati ya 14 yanayoshiriki zoezi hilo, lakini upigaji kura unaendelea katika majimbo mawili muhimu sana, Texas na California, ikimaanisha kuwa atakayeibuka na ushindi mkubwa kabisa usiku huu bado hajulikani.
Ushindi wa makamu wa rais wa zamani Biden katika majimbo hayo yenye Wamarekani weusi wengi umeingiana na ushindi wa mwishoni mwa wiki katika Jimbo la South Carolina.