Rais wa Marekani Joe Biden ameshiriki kwenye mkutano wa Munich wa masuala ya usalama uliofanyika kwa njia ya video, ambapo katika hotuba yake ameahidi Marekani itashirikiana na washirika wake wa Ulaya katika juhudi za kukabiliana na changamoto zilizopo, ikiwa ni pamoja na janga la maambukizi ya Corona, ugaidi na mabadiliko ya tabia nchi.
Biden amesema kuwa suala la mabadiliko ya nchi ni suala linalohusu uhai wa binadamu wote na kwa ajili hiyo ameirudisha Marekani kwenye mkataba wa Paris juu ya mabadiliko ya tabia nchi.
Kuhusu janga la Corona, Biden amesema ushirikiano wa dunia nzima unahitajika katika juhudi za kukabiliana na janga hilo na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua kabambe ambapo Marekani itatenga kiasi cha dola bilioni 4.5 kwa ajili ya kuunga mkono mpango wa chanjo kwa manufaa ya nchi masikini.
Kansela Angela Merkel na Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen pia wametangaza kutoa fedha zaidi ili kuchangia katika mpango wa chanjo, maarufu kama COVAX ambapo Merkel amesema Ujerumani itaongeza Euro bilioni 1.5.
Viongozi wengine walioshiriki kwenye mkutano wa Munich kwa njia ya video ni pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Mwenyekiti wa zamu, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson.
Halmashauri ya Umoja wa Ulaya nayo itaongeza mchango wake kutoka Euro milioni 500 hadi Euro bilioni 1.5, fedha ambazo zitatolewa kwa nchi masikini kama msaada na mikopo.