Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza muelekeo mpya wa sera za nje za nchi yake, akijaribu kujiondoa kwenye njia ya uhasama na kujitenga iliyofuatwa na mtangulizi wake, Donald Trump.
Akitangaza kile alichokiita kurejea rasmi kwa Marekani kwenye uwanja wa diplomasia ya kilimwengu, Biden amewaambia wanadiplomasia kwenye Wizara ya Mambo ya Kigeni ya nchi yake kwamba wana jukumu kubwa la kurekebisha mambo yote yaliyovurugwa yanayohusisha taswira ya Marekani duniani.
Biden ametumia hotuba hiyo kuonesha utayari wa serikali yake kuhakikisha kuwa Marekani inasimama imara mbele ya mahasimu wake wa jadi, Urusi na China lakini kwa njia ambazo hazitahatarisha mataifa mengine.
Aidha Biden ametangaza kusimamisha uungaji mkono wa nchi yake kwa vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen, akisema hiyo ni hatua mojawapo ya msimamo wa Marekani kuhimiza diplomasia, demokrasia na haki za binaadamu duniani kote.
Hotuba hiyo ya Biden imeeleza pia msimamo wa Marekani dhidi ya mapinduzi ya kijeshi ya Myanmar, ambapo alitaka kurejeshwa mara moja kwa utawala wa kiraia.